Breaking News

Ray C afunguka kuhusu utumwa wa Dawa za kulevya....akanusha kutoka kimapenzi na JK...!

  1.   GWIJI wa muziki wa Bongo Flava,   Rehema Chalamila, al-maarufu Ray C amekanusha vikali uvumi ambao umekuwa ukisambaa Tanzania na Afrika Mashariki kwa jumla kwamba amewahi kuwa na urafiki wa kimapenzi na Rais Jakaya Kikwete wa Tanzania.
Hata hivyo, Ray C, alikiri jinsi alivyookolewa na Rais Kikwete kutoka katika janga la mihadarati baada ya rais huyo kupata habari zake katika vyombo vya habari. Msanii huyo ameanzisha kituo cha kuwafanyia marekebisho waathiriwa wa mihadarati ambao wengi wao ni vijana.

Swali: Uliingiaje katika matumizi ya mihadarati?
JIBU:  Mpenzi wangu wa zamani aliniingiza katika janga hili. Sikujua mapema kwamba alikuwa mraibu wa mihadarati nilipokutana naye kwanza. Wala sikujua tofauti ya bangi na mihadarati mingine kutokana na ugeni wangu. Polepole nilijikuta nikitumia dawa za kila aina. Mwili wangu ulianza kudhoofika huku nikishindwa kukaa bila kutumia mihadarati. Mwili wote ungeniuma kama ningekosa kutumia.

Swali: Unakumbuka ulitumia kiasi gani cha pesa kwa wiki katika hiyo mihadarati?
JIBU: Kilikuwa kiasi kikubwa mno ambacho siwezi kukikumbuka. Machozi hunilengalenga kila ninapojaribu kukumbuka. Wakati mmoja ilinibidi kuuza nyumba yangu, nikafunga maduka na kuuza mali yangu nyingi ili nipate pesa za mihadarati. Nilijifunza kwamba haijalishi kwamba u tajiri kiasi gani. Ukijiingiza katika matumizi ya mihadarati lazima hatimaye ufilisike.

Swali:Je, familia yako ilijua kuwa ulikuwa umetumbukia katika janga la matumizi ya mihadarati?
JIBU: Nilijaribu sana kujificha nikitaraji kuwa hali yangu haingetambulika. Hata hivyo, mamangu alitambua mabadiliko niliyokuwa nayo. Sura yangu haikung’ara tena, nikapoteza hamu ya kula na zaidi ya hayo nilikuwa mwepesi sana wa kukasirika. Mama aliniita na kunishauri kuukata urafiki na mpenzi wangu ambaye alimjua kama mzoefu wa kutumia mihadarati lakini nikapuuza ushauri huo.

Swali: Uliamua lini kuacha matumizi ya mihadarati?
JIBU:  Ulikuwa mwaka 2012 ambapo niliamua ama nijiue au niende jela. Nilikuwa nimechoshwa na utumwa wa mihadarati. Sikuona maana ya maisha ikiwa kila senti niliyoipata iliingia katika mihadarati. Niliachana na mpenzi wangu. Kama mamangu hangekuwepo kunishughulikia sasa hivi stori ingekuwa tofauti.

Swali: Je, uliweza kuacha matumizi hayo ya mihadarati tu ghafla kama umepunguza tu kama watu wasemavyo?
JIBU:  Wajua watu wanayo mengi sana ya kusema na huwezi kuwazuia. Rais Kikwete alipojitolea na kunisaidia nilijikaza kisabuni na kuachana na mihadarati. Nilitaka kuachana na aibu yangu ya kutajwatajwa hadharani kama mwathirika wa matumizi ya mihadarati na Mola ameniwezesha kufikia lengo langu.

Swali: Je, Rais Kikwete alijuaje shida yako na kunao ukweli wowote kwa mlikuwa na urafiki wa kimapenzi?
JIBU: Sina hakika sana ila nakisia tu kwamba ilikuwa kupitia katika vyombo vya habari hasa magazeti na radio baada ya mamangu kuzungumza na waandishi wa habari. Kuhusu urafiki hilo nakanusha kabisa kwa maana ilikuwa mara yangu ya kwanza kumwona akiwa karibu nami na ninamshukuru sana kwa ukarimu wake ambao umeniweka hai hadi leo. Nitamwombea Mungu ambariki katika kila alifanyalo.

Swali: Je, kumekuwa na mabadiliko yoyote kwako tangu uache mihadarati?
JIBU: Sasa ninaishi maisha ya uhakika. Najisikia kuwa mwenye afya. Lakini sina imani tena na wanaume na nitakaa kwa muda bila kuwa na urafiki nao na ikiwa ni lazima urafiki huo uwepo basi nitamtafuta mwanamume wa miaka 60 na zaidi. Sitataka urafiki na vijana tena kwani huo ndio ulioniingiza katika mateso niliyopitia.

Swali: Umekaa miaka kadhaa bila kuwa katika ulingo wa muziki. Huoni kuwa umesahaulika?
JIBU:  Umahiri wangu nauona uko pale pale. Ni kweli kuna mabadiliko makubwa na mazuri katika muziki chapa Bongo Flava. Hata hivyo, kwa vigogo kama sisi tunasalia pale pale; tunaona wageni wakija na kupita kama moshi tu huku sisi tukisalia pale pale tukiendelea kuimarika tu. Tayari nimetayarisha albamu mpya na nasubiri wakati mwafaka kuizindua.

Swali: Umefungua kituo cha Ray C Foundation kusaidia walioathiriwa na mihadarati. Je, unatarajia kumsaidia mpenzi wako wa zamani pia?
JIBU: Ni hiari yake. Siwezi kumlazimisha. Ni vigumu sana kumlazimisha mtu kubadilisha mwenendo wake. Hata hivyo, akija nitakuwa tayari kumpokea na kumsaidia.

Swali: Je, ni kweli wanavyodai mashabiki wako kuwa umeichubua ngozi yako ili uonekane mweupe zaidi?
JIBU:  Hata kidogo na wala sidhamirii kufanya hivyo karibuni. Kunawiri kwa ngozi yangu kwatokana na afya nzuri ambayo imeanza kurudi hivi karibuni.

Swali: Tumekaa sana bila kitu kipya kutoka kwako. Unatupa nini hivi karibuni?

Jibu: Tayari nimerekodi albamu mpya ingawa meneja wangu anasisitiza tusubiri hadi wakati mwafaka uwadie ndipo tuachilie ngoma hizo. Nina hakika mtazifurahia

No comments