Breaking News

MAKUBWA HAYA: WAUGUZI WAIKIMBIA HOSPITALI KISA UCHAWI

SERIKALI ya Kaunti ya Elgeyo Marakwet  inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuwatuma wafanyakazi katika kituo cha afya cha Simbeiwe, kaunti ndogo ya Marakwet Magharibi, baada ya wahudumu wa afya wanaotumwa hapo kukataa kazi kwa kuhofia uchawi eneo hilo.
Kumekuwa na imani kwamba eneo hilo ni kitovu cha uchawi katika kaunti huku wafanyakazi wakipata habari za kuogofya kwamba mazimwi pia hutafuta matibabu katika kituo hicho.

Mmoja wa wauguzi aliyeacha kazi katika kituo hicho aliripotiwa kutibu 'zimwi’ la kike ambalo lilifanya muujiza kwa kuning’iniza mtoto mdogo hewani, bila kumshika, mbele ya muuguzi huyo ambaye alikuwa akijitayarisha kumdunga sindano.

Waziri wa Afya katika kaunti hiyo, Bw Thomas Ruto alisema idara yake inatafuta wahudumu wa afya ambao wanaweza kustahimili kazi katika mazingira kama hayo.

Lakini Mwakilishi wa Wadi ya Moiben-Kuserwo William Chesing’any, alipuuza madai hayo akisema kuwa uchawi uliendeshwa na kizazi cha zamani ila kwa sasa haupo.

“Imani hiyo inaendelea kufifia. Sasa tuna watumishi wa umma ambao ni pamoja na walimu wanaofanya kazi Simbeiwet na Mindiliwo. Desturi hiyo inastahili kusahaulika,” alieleza.

Kwingineko, mhudumu mwanamume katika kaunti hiyo amechukuliwa hatua kwa kuhamishwa kufuatia madai kuwa alitaka kuwa na uhusiano wa kimapenzi na wagonjwa wake.

Hii inafuatia hatua ya wakuu katika lokesheni ndogo ya Kapcherop, Marakwet Magharibi, kupiga marufuku wanawake wote na wasichana kutafuta huduma za kimatibabu katika dispensari inayosimamiwa na mhudumu huyo anayetajwa kama mtundu.

Wakuu wa kaunti pia wanatazamia kuchukua hatua zaidi dhidi ya mhudumu huyo ambaye amedaiwa kutaka kutoa huduma za ziada kando na zile ambazo wagonjwa wa kike wanatafuta.

Marufuku yao ilifuatia malalamishi kutoka kwa wagonjwa wa kike kwamba mhudumu huyo alikuwa na mazoea ya kuwapapasa sehemu zao za siri akiwa anawahudumia hata kwa maradhi kama mafua.

“Hata wakati mtu akitaka matibabu ya mafua, yeye angempapasa kwa mkono wake kuanzia shingoni hadi kwa mapaja kupima joto la mwili,” mmoja wa wakazi alilalamika.

Kudhihirisha madai
“Mwanamke aliyetumiwa na viongozi kutafuta matibabu katika kituo hicho ili kudhihirisha madai hayo, alithibitisha tabia ya muuguzi huyo, ambaye alijaribu kumwandama kingono na nia nyinginezo ambazo hatuwezi kueleza,” alisema Bw Ruto.

Viongozi hao pia walibaini kuwa kituo hicho kimetorokwa na wakazi wa kike ambao wameshauriwa na waume wao na wazee wa kijiji wasisogee karibu na mhudumu huyo.

Dawa kadhaa zilizoharibika pia zilipatikana katika kituo hicho.
Afisa mkuu wa afya katika kaunti, Bi Caroline Magut alitaja tabia ya mfanyakazi huyo kama isiyoamabatana na maadili, kukosa utaalamu na pia ya kushangaza.
“Tumechukua hatua ya kinidhamu na kwa sasa tunaendelea kumfuatilia kwa karibu. Tumemhamisha hadi katika kituo chenye shughuli nyingi huku mipango ya kumuondoa kazini ikitayarishwa,” alisema Bi Magut

No comments