Breaking News

SOMA MIKAKATI YA UKAWA YA KUING'OA CCM MADARAKANI MWAKA HUU 2015


Mwenyekiti wa taifa chama cha demokrasia na maendeleo (Chadema), Mh. Freeman Mbowe amesema njia pekee ya kukiondoa chama cha mapinduzi madarakani katika uchaguzi mkuu ujao ni viongozi wa vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi (Ukawa), kuweka kando maslahi binafsi ya vyama vyao na kusimamisha mgombea mmoja katika kila nafasi ya uongozi, huku akionya kuwa endapo atatokea kiongozi yeyote ndani ya Ukawa mwenye uchu wa madaraka ni afadhali akatengwa kama msaliti.

Akihutubia maelfu ya wakazi wa manispaa ya Tabora katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Town School, kata ya gongoni mjini Tabora, mwenyekiti huyo mwenza wa Ukawa, amesema mambo yaliyojitokeza wakati wa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa baadhi ya wagombea wa vyama vinavyounda Ukawa, ambavyo ni Chadema, CUF, NCCR – mageuzi na NLD kugombania baadhi ya maeneo kwa ajili ya tamaa na uchu wa madaraka yanapaswa kuwa ni funzo kwa uchaguzi ujao wa mwezi oktoba mwaka huu.
Mh. Mbowe ambaye pia ni kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani bungeni na mbunge wa hai, ameeleza kusikitishwa na hali ya umaskini inayowakabili wakulima wa mazao mbalimbali nchini, wakiwemo wa zao tumbaku mkoani Tabora na pamba katika mikoa ya Mwanza, Mara, Shinyanga na Simiyu kutokana na kulipwa bei ndogo jambo ambalo limesababisha hata baadhi ya viwanda vya nguo nchini kufa kifo cha kawaida, huku serikali ikishindwa kuvifufua na badala yake imeendelea kukaribisha wawekezaji wa nje kuja nchini kuwekeza kwenye migodi ya madini na wananchi kuambulia mashimo.

Kwa upande wake, naibu katibu mkuu wa Chadema Zanzibar, Salum Mwalimu amesema kwamba kwa muda mrefu watanzania wamekuwa wakidanganyika kwa kudhani kuwa uongozi mbovu ni matokeo ya viongozi waliowachagua na kusahau kuwa tatizo sio viongozi wanaotokana na chama cha mapinduzi, bali ni chama chenyewe, dhamira yake na mifumo waliypoiweka katika kutumikia watanzania.

No comments