Breaking News

UNDANI WA AJALI YA IRINGA: BASI LAUA ZAIDI YA ABIRIA 40 BAADA YA KUANGUKIWA NA KONTENA CHANGARAWE MAFINGA


AJALI mbaya ya gari imetokea asubuhi ya jana saa 3.30 Jumatano katika kijiji cha Changarawe wilayani Mufindi mkoani Iringa baada ya basi la abiria la kampuni iitwayo Majinja lililokuwa likitokea Mbeya kuelekea Dar es Salaam, kugongana na lori la mizigo lililokuwa likitokea Dar kuelekea Mbeya na kusababisha vifo vya watu wanaokadiriwa kufikia 42 na majeruhi 22.

Habari kutoka eneo la tukio, zinasema ajali hiyo ilitokea wakati lori hilo lililokuwa limepakia kontena, likiwa katika mwendo wa kasi, lilipojaribu kulikwepa shimo lililokuwa katikati ya barabara na lilipotaka kurudi upande wake, ndipo lilipogongana uso kwa uso na basi hilo, linalokadiriwa kuwa na zaidi ya abiria 50 ndani yake.

“Hili lori lilipogongana na basi, kontena lake likaliangukia basi kiasi kwamba abiria wote wamelaliwa, watu wengine wanadaiwa walirushwa katika korongo kufuatia kishindo cha mgongano.
Hali ya kuwaokoa maiti na majeruhi ni ngumu kwa sababu hakuna gesi ya kukatia vyumba hapa Mafinga,” alisema shuhuda mmoja wa ajali hiyo ambaye hakutaja jina lake.

Watu ni wengi eneo la tukio na miongoni mwa viongozi wa serikali ni pamoja na Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Amina Juma Masenza.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Ramadhani Mungi ambaye pia yupo eneo la tukio hivi sasa, amewasiliana nasi na kuahidi kutoa ushirikiano zaidi baadaye kwa vile hivi sasa hekaheka ni nyingi.
 
Maiti nane watambuliwa
WATU wanane kati ya 42 waliofariki katika ajali ya gari iliyotokea asubuhi leo katika kijiji cha Changarawe, huko Mafinga wametambuliwa kufuatia zoezi linaloendelea katika hospitali ya Mafinga ambako miili ya marehemu imelazwa.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi ameuambia mtandao huu hivi punde kuwa ajali hiyo iliyohusisha lori aina ya Scania, lenye namba ya usajili T 689 APJ lililokuwa likiendeshwa na Maiga Sebastian na basi la abiria T 338 CBE, ambalo dereva wake alikuwa Baraka Godbless, ilitokea baada ya lori hilo kuliovateki lori lingine la mafuta lililokuwa mbele yake katika mteremko mkali.
 
“Magari yote mawili yalikuwa yanashuka katika mteremko mkali, lori likitokea Mafinga na basi likitokea Makambako, lori baada ya kuovateki, likaona shimo barabarani, katika kulikwepa akahamia upande wa basi, yakagongana uso kwa uso. Lakini pia kontena lililokuwa kwenye lori, likiwa na vitu vizito, likalilalia basi katikati,” alisema Kamanda.

Akifafanua, alisema katika idadi ya vifo hivyo, watu sita walikuwa wanawake na 36 wanaume, wakiwemo watoto watatu huku majeruhi wakiwa ni 22. Zoezi la kutambua maiti bado linaendelea na kwamba kwa sasa hawezi kutaja majina ya waliotambuliwa.

(HABARI: OJUKU ABRAHAM/GPL)

No comments