Breaking News

NEWS Ukaguzi wa wanafunzi hewa ufanyike haraka

   WIKI iliyopita Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, aliwaagiza wakuu wa wilaya na maofisa elimu, wafanye ukaguzi katika shule zote nchini ili kubaini wanafunzi hewa kwenye mpango wa elimu bure.
Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, kila mwezi Serikali inapeleka kwenye shule zaidi ya Sh bilioni 18 kugharamia elimu bure, lakini sasa udanganyifu umeanza kujitokeza katika mpango huo kwa kuwa na wanafunzi hewa.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo, alipokutana na watumishi na viongozi wa Manispaa ya Ilala katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam. Majaliwa anataka wakuu wa wilaya na maofisa elimu, kwenda kufanya ukaguzi ili kupata takwimu sahihi.
Anasema wakuu wa wilaya na maofisa elimu, wakiona takwimu zinawachanganya, ni lazima watoke ofisini kwenda katika shule zilizo kwenye mpango wa elimu bure, kufanya uhakiki wa idadi ya wanafunzi.
Tunahimiza wakuu hao wa wilaya na maofisa elimu, kutekeleza haraka agizo hilo la Waziri Mkuu kwa kupitia shule zote bila kuacha yoyote. Tunasema hivyo, kutokana na ukweli ulioanza kubainika katika maeneo mengi nchini, kwa mfano wilaya ya Ilala Mkoa wa Dar es Salaam.
Katika taarifa yake, Mkuu wa Wilaya hiyo, Sophia Mjema anasema hajaridhika na uhakiki wa wanafunzi hewa uliofanyika; na anaamini wapo wanafunzi wengi hewa, hivyo ameagiza uhakiki ufanywe upya ili kujua idadi iliyokamilika.
Anasema uhakiki wa awali umeonesha wilaya ina wanafunzi hewa 599, lakini alipopitia kwa kina alibaini kuwa wanafunzi hao hewa, wapo katika shule za msingi sita tu, kati ya 99, wilayani humo.. Kwa sasa maofisa elimu na wakuu wa shule wilayani humo, wameagizwa kuhakiki kwa mara ya pili ili kujua kama ni kweli wapo wanafunzi hao tu au zaidi katika shule hizo.
Tunampongeza Mjema kwa hatua yake hiyo ya kutoridhishwa na idadi hiyo aliyokabidhiwa. Tunataka wakuu wengine wa wilaya, wasiridhike na idadi wanayopelekewa. Wakuu wengine wa wilaya wanatakiwa kuiga mfano huo wa Ilala, kwa kufanya uhakiki zaidi ya mara moja hadi kumaliza shule zote.
Tunahimiza uhakiki huo ufanywe kupitia fomu maalumu, watakazojaza pia wanafunzi, kama fomu zile wanazojaza wanapoingia darasa la kwanza. Tunalaani uwepo wa wanafunzi hewa mashuleni na tunashutumu walimu wakuu wote wanaopika takwimu ili kujipatia fedha za mpango wa elimu bure.
Hatukutarajia walimu wakuu wa shule, wangechakachua takwimu hadi kuonesha wana wanafunzi wengi, wakati idadi iliyopo shuleni ni tofauti. Walimu wa aina hiyo wenye lengo la kutumia fedha za walipa kodi kwa maslahi yao binafsi, wanatakiwa kuchukuliwa hatua kali.
Tunashauri wakuu wa wilaya na wakurugenzi, wahakikishe kuwa hadi Septemba mosi mwaka huu, wawe wamepata idadi kamili ya wanafunzi hewa katika wilaya zao; na wakamate walimu wote waliopika takwimu za mpango huo wa elimu bure

No comments