Breaking News

MAJANGA: NYOKA KUFIKISHWA MAHAKAMANI KAMA USHAHIDI

NYOKA aliyepatikana katika nyumba ya mshukiwa wa ulaghai jijini Nairobi, atatolewa kortini kama ushahidi kama mahakama ilivyoagiza.
Upande wa mashtaka ulisema kuwa uko tayari kuwasilisha nyoka huyo kesi dhidi ya raia wa Congo, Mangili Kayeba itakaposikilizwa Machi 24 mwaka huu.

Mahakama iliambiwa kuwa mnyama huyo anazuiliwa katika hifadhi ya wanyama ya Nairobi na ametaka mayai tangu apelekwe huko mwaka jana.

Hakimu Mwandamizi wa Kibera Bw Tito Gesora, aliagiza upande wa mashtaka kufikisha nyoka huyo kortini  ili kudhibitisha kesi dhidi ya Kayeba

Polisi walidai walimpata nyoka huyo katika chumba kimoja walipokuwa wakifanya uchunguzi katika nyumba ya Kayebe iliyoko eneo la Kilimani jijini Nairobi.

Inashukiwa kuwa mshtakiwa alikuwa akimtumia nyoka huyo kufanya vituko vya ushirikina kwa kuwapumbaza watu aliolenga kuwalaghai.

Polisi walienda katika nyumba yake kufanya msako baada ya kumkamata akiwa na pesa bandia. Walimshtaki kwa kupatikana  akifuga mnyama kinyume cha sheria za kulinda wanyamapori nchini mashtaka ambayo Kayeba alikanusha.

Kulingana na sheria, ni makosa kwa  mtu kupatikana akifunga mnyama wa porini bila kuwa na kibali kutoka kwa shirika la kutunza wanyama pori nchini.

Aidha, Bw Kayebe alishtakiwa kwa kupatikana na pesa bandia akiwa na nia ya kufanya uhalifu. Kesi yake  imepangiwa kuanza Machi 24 mwaka huu.

Bw Gesora alisema ni lazima upande wa mashtaka uwasilishe mahakamani ushahidi ulio nao dhidi ya mshtakiwa ikiwa na pamoja na nyoka huyo.

Wakati huo huo, mwanamume aliyepatikana akitumia  cheti cha mtihani wa kidato cha nne na kitambulisho cha mtu mwingine akiomba kazi, alijipata pabaya aliposhtakiwa kwa wizi.

Upande wa mashtaka ulisema kwamba James Butali, aliiba vyeti hivyo kutoka kwa Bw Joseph Kaptut ambaye nyumba yake ilivunjwa mnamo Machi 9 mwaka huu mtaani Kawangware, Nairobi.

Kuvunja nyumba
Butali alishtakiwa kwa kushirikiana na watu wengine ambao hakuwa kortini kuvunja nyumba ya Bw Kaptut eneo la Kawangware ambapo ilidaiwa  aliiba vyeti hivyo na nguo ikiwemo jezi iliyokuwa na maandishi na nebo ya timu ya soka ya Chelsea.

“Ulipatikana na jezi iliyokuwa na nebo ya timu ya soka ya Chelsea ukijua kwamba ilikuwa mali ya wizi au ukiwa umeiba,” shtaka lilisema.

Kulingana na mashtaka, aliwasilisha  cheti na kitambulisho cha Bw Kaptut kwa kampuni moja kuomba kazi na ndipo ikagunduliwa havikuwa vyake.

Hata hivyo, alikanusha mashtaka akisema kwamba yeye ni shabiki damu wa Chelsea na haikuwa mara yake ya kwanza kuvaa jezi hilo.

Hakimu Mkuu wa Kibera Bi Judith Wanjala, aliagiza upande wa mashtaka kumkabidhi mshtakiwa nakala zote za ushahidi kabla ya Juni 12 kesi itakaposikilizwa.


Alimwachilia kwa dhamana ya Sh50,000 na mdhamini wa kiasi hicho

No comments