Mjamzito Afariki Baada Ya Kuangukiwa Na Mti Korogwe
Ndugu wawili akiwemo mwanamke mwenye ujauzito wa miezi saba, wamefariki dunia katika kijiji cha Zege kata ya Dindira wilayani Korogwe, wamekufa papo hapo na wengine wawili kujeruhiwa vibaya baada ya kuangukiwa na mti wakati wakitafuta kuni msituni.
Waliokufa kutokana na kuangukiwa na mti aina ya msambu ni Mariam Saidi (17), mwanafunzi wa kidato cha nne katika Sekondari ya Dindira na Selina Saidi (29) aliyekuwa mjamzito.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Juma Ndaki alithibitisha kifo hicho na kusema kilitokea mwishoni mwa wiki wakati wanawake wane, ambao ni ndugu wa familia moja walipokuwa wakikata kuni kwenye msitu wa Sakale, jirani na kijiji chao.
Alitaja waliojeruhiwa kwenye tukio hilo kuwa ni Zubeda Seif (19) na Batuli Saidi (15), ambaye naye ni mwanafunzi wa shule ya sekondari ya Dindira.
“Siku hiyo ya tukio wanawake hao wanne waliingia msitu wa Sakale kwa lengo la kukata kuni na wakati wakiendelea na shughuli hiyo bila kujua kumbe walikuwa chini ya mti mkubwa wa Msambu ambao ulikuwa umeshakauka siku nyingi,” alisema.
Alisema uchunguzi wa awali, umeonesha kuwa mizizi ya mti huo, ilishakauka siku nyingi na kufikia hatua ya kulegea, kiasi cha kuyumba na kuwaangukia wakati huo walipokuwa wakiendelea kukata kuni chini yake.
“Inaonyesha tukio la kuanguka kwa mti huo, lilikuwa la ghafla sana na hivyo kusababisha Selina na Mariam kushindwa kukimbia ili kujinusuru, hasa baada ya miili yao kufunikwa kabisa na mti huo”,alisema.
Aliongeza “Kitendo hicho kilisababisha Mariam kupasuka kichwa papo hapo na Selina ambaye alikuwa mjamzito naye kupoteza maisha yake na ya mtoto tumboni…kwa bahati Zubeda na Batuli wao walifanikiwa kukimbia lakini matawi ya mti huo yaliwapiga na kuwajeruhiwa maeneo tofauti tofauti ya mwili,” alisema.
Hata hivyo, Ndaki alisema majeruhi hao wamelazwa katika Kituo cha Afya cha Bungu kwa matibabu na kwamba hivi sasa hali ya afya zao zinaendelea vizuri.
No comments